NILIWAHI KUANDIKA MAKALA HII HAPA OCTOBER 2013 JUU YA NGUVU KUBWA WANAYOTUMIA MATAIFA YA MAGHARIBI KUPITIA MWAMVULI WA ICC NA UHUSIANO WAO NA UKOLONI MAMBO LEO. TUJIKUMBUSHE HAYA: | Gossip Wire
Breaking News
Loading...

Saturday, April 26, 2014

NILIWAHI KUANDIKA MAKALA HII HAPA OCTOBER 2013 JUU YA NGUVU KUBWA WANAYOTUMIA MATAIFA YA MAGHARIBI KUPITIA MWAMVULI WA ICC NA UHUSIANO WAO NA UKOLONI MAMBO LEO. TUJIKUMBUSHE HAYA:

AFRICA NA UKOLONI MAMBO LEO NA ICC: KWANINI AFRICA?
Maisha ya binadamu hayajawahi kuwa maraisi au mepesi. Kila mmoja hupambana ili kuweza kuyamudu. Kuna njia nyingi za kupambana ila moja kubwa inayotumiwa na mabepari (capitalist)  ni kunyonya mataifa dhaifu (maskini). Hutumika kila njia ikiwezekana kuhatarisha maisha ya maskini ili kujinufaisha. Utu kwa bepari ni nadharia tu. Kwani hutunga chochote kile kulinda nafsi yake (status) katika Dunia.
            Waliamua kuitawala Africa ili kuweza kupata malighafi kwa ajili ya viwanda vyao pamoja na soko la bidhaa zao kutokana na ushindani uliokuwepo. Hapa walikuja kama wamisionari, wafanyabiahsara na wanajiografia. Hayo yote yalikuwa ni mwamvuli tu. Bali lengo kuu ni unyonyaji wa nguvu kazi ya Africa na rasilimali za Africa.
            Waafrica wenzangu, tutambue ukoloni ulikufa na sasa wanatumia ukoloni mamboleo. Mimi huita scientific colonialism, hutumia uwezo wao wa sayansi na teknolojia katika kutimiza  adhima yao ya kuzitumia rasilimali za Africa na wanatumia njia zozote za kuvuna rasilimali hizi pasipo Africa kujielewa. Kuna njia nyingi ila moja ni kuwathibiti viongozi hawa wa Africa ambao wamekuwa wazalendo kwa Nchi zao na hawautaki ubeberu wao. Basi viongozi hawa hudhibitiwa kwa njia mbili:
            Moja ni kwa mapinduzi ya waasi, hili mataifa haya huwafadhili waasi kwa siri sana, ili kuziondoa serikali hatarishi uongozini wapate upenyo wa kuendeleza unyonyaji (Divide and rule).
            Pili ni hii mahakama ya ICC (The Hague). Hutumia mahakama hii kama fimbo ya kuwaadabisha viongozi wa kiafrica. Rais wa Libya asingekufa angekuwa the Hague, vivyovivyo kwa Misri, Sudan na sasa ni Kenya. Africa lazima tuungane katika hili kwani leo ni Kenya kesho Uganda, Tanzania, Malawi na hata Africa kusini pale tutakapokuwa ukuta kuzuia unyonyaji wao.
            Ndipo swali hili linakuja kwa nini Africa? Ni swali kila mzalendo wa Africa atajiuliza, kwa nini Afrika! Na sio Ulaya, Amerika, Australia na Asia? Je, umoja wa mataifa ni kwa ajili ya Afrika pekee?
            Ijumaa ya tarehe 10/10/2013 Nchi wanachama wa umoja wa Africa watakutana mjini Addis Ababa mada kuu ikiwa ni mahusiano ya Africa na ICC. Shukran kwa Kaguta Yoweri Museven. Suala hili linaumiza kichwa diplomasia ya Ulaya na America huku ikiwa kama panaweza kutokea shinikizo la Nchi wanachama wa umoja wa Africa kujitoa katika mkataba wa Rome.
            Waafrica wenzangu, ni lazima tujiulize maswali juu ya uwepo wa ICC na utendaji wake ndani ya Africa. Kwanini ni viongozi wa kiafrica tu ndio wanao kwenda The Hague? Je! Wanataka kutuambia kuwa mataifa  ya Magharibi hawakiuki haki za binadamu? Tujiulize kuhusu alichokifanya George W. Bush kule Iraq na Pakistan, walichokifanya umoja wa Ulaya na Marekani(Obama) kule Libya. Je, hii haitoshi kuwashitaki nao wakaenda The Hague? Kwa nini Afrika?
            Wafrika wenzangu, tumekuwa wanyonge sana na tumekosa umoja ya kusema sasa inatosha kwa udhalimu huu wa ICC. Tafadhali viongozi wan chi wanachama wa umoja wa Afrika mkutanapo tar 10/10/2013 muwe na sauti moja yenye maamuzi magumu itakayoitikisa Dunia na kuifikishia ujumbe kuwa udhalimu na unyonyaji huu umetosha, umefika kikomo
            Nionavyo ni vyema umoja wa Africa ukawa na mahakama yake ili kuweza kuyamaliza mambo ya ndani ya Africa, kwani tuna tamaduni zetu za kumaliza mizozo, na tuna tamaduni zetu za kusuluhishana. Haina haja ya ICC kuendeleza udhalimu huu Afrika. Tuungane pamoja katika maamuzi ya kujenga Africa madhubuti.
            Sio hivyo tu, bali najiuliza pia mahakama hii ilianzishwa kwa misingi gani? Nani walikuwa walengwa? Kuna nini nyuma ya mahakama hii? Tuangalie zaidi ya kikomo cha macho yetu yaonapo. Naamini kwa mwendo wa ICC, basi ni dhahiri kuwa ni fimbo ya kuiongoza Africa katika kuimarisha na kusimika mizizi ya ubepari Africa.
            Tumewahi kujiuliza ni nani anayewafadhili waasi Africa? Je ni kweli huitaji kuingia madarakani kwa demokrasia tena walioileta wao wenyewe ? wao wenyewe tena husaidia waasi kuingia madarakani? Ni dhahiri kuwa kuna tusichokiona hapa. Nani anayegharamikia silaha wanazotumia waasi?, ni nani aliyenyuma yao? Kwa mfano wa Libya, ni nani aliyewaandaa waasi katika kumwangusha simba wa Africa aliyekuwa adui mkubwa wa Amerika? Lazima  tukubali yaliyotokea Libya haikuwa ridhaa ya wanalibya bali kuna siri nzito nyuma yake. Kwanini Afrika?
            Waafrica wenzangu haya yote yanayofanyika na wabepari hatuyaoni? Kwa nini tuwahukumu waafrica wenzetu? Kwa nini tutumike kama chombo cha kuiangamiza Africa yetu kwa faida ya wabepari? Kwa nini tufanywe wajinga na wavivu wa kufikiri kiasi hicho. Tuseme imetosha, pamoja tujenge Africa mathubuti.
Mazingira ya machafuko ya kisiasa Afrika huziandaa wenyewe kwa agenda zao za siri kisha wanakuja kutuadhibu na chombo hichi, mahakama ya ICC.Nataka tuelewe kuwa mbali na mahakama hii viongozi wengi wa Africa huwekwa madarakani wakiwa wameandaliwa kutimiza matakwa ya mabepari. Viongozi wengi wa Africa ni mapandikizi ya mabepari yanayoiangamiza Africa yao wenyewe ndio maana hawana maamuzi ya umoja.
Funguka Africa, ICC ni kiini macho tu, kuna mengi nyuma ya pazia. Tuukatae ukoloni mamboleo ulioshika mizizi. Tuwe wamoja kujenga Africa mathubuti, tusipigane wenyewe kwa wenyewe, tukatae kuwa mashabiki wa magharibi. Tujifunze kwa Libya walivyoishabikia America, Nato na waasi pasipo kujua kuwa wanajiangamiza wenyewe. Je divide and rule haijatunga kazi kule Libya? Marekani alichukua tani ngapi za matuta? Fikiri kwa nini Afrika?
Waafrica wenzangu, tuache ushabiki wa kisiasa ulio na hisia za kipandikizi pasipo kujijua, tutaiangamiza Africa sisi wenyewe.Historia imetuweka tulipo lakini isiendelee kututafuna na kuturudisha nyuma. Tufunguke kifikra, tujenge mshikamano na umoja madhubuti. Tufanye kazi kwa bidii na kutumia fursa zilizopo katika kujiajiri. Zaidi sana tujenge Africa bora, jasiri na madhubuti yenye kulinda rasilimali zake kwa manufaa ya watu wake.
Tuwe na sauti moja Africa tuupinge ukoloni mamboleo, historia isijirudie, kila mmoja anajukumu la kuijenga Africa mathubuti,. Marais wa Africa tarehe 10/10/2013 muwe na sauti moja mathubuti yenye tija kwa Africa. Msiogope ijengeni historia mpya Afrika. Pamoja tuijenge Afrika madhubuti.
             Imeandikwa na Faraja Simon
            Email: farajasimon@yahoo.com, farajasimonm@gmail.com

            mobile: +255787539392, +255763222443

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT